Naam! Haya
ninayosema yanaweza kuonekana kama ndoto kwa wengine, lakini kwangu mie ni
faraja kubwa na mwanzo wa nuru mpya katika siasa za Tanzania. Itakapofika siku
hii, Tanzania itaandika historia nyingine mpya katika kuelekea kwenye
demokrasia ya kweli. Ni siku ambayo siasa za Tanzania zitapata wokovu mpya.
Naam, hii ni siku Halima Mdee, mbunge mwanamke na kijana toka jimbo la Kawe, atakapochaguliwa kuwa Kiongozi wa kambi rasmi
ya upinzani bungeni.
Naamini kwa
baadhi ya wasomaji wangu bado hawajaelewana vema ni nini ninachokimaanisha kwa
kauli yangu hii. Bila shaka unaweza kudhani nimetoa fumbo Fulani hapa. Lakini
nakuhakikishia hakuna fumbo. Ni nini basi kimenisukuma kuandika haya kwenye
ukurasa huu leo? Ngoja nikueleze.
Alhamisi
ijayo, yaani Oktoba 27, chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini kiitwacho
Democratic Alliance (DA), kitafanya uchaguzi wa kiongozi wa kambi rasmi ya
upinzani bungeni. Wanaowania nafasi hiyo ni wawili; Bw. Athol Trollip (47)
pamoja na Bi. Lindiwe Mazibuko (31).
Bw Trollip
ambaye ni mzungu, ndie kiongozi wa sasa wa kambi ya upinzani bungeni
anayemaliza muda wake, na amekuwa katika nafasi hiyo tangu mwaka 2009. Pia ni
kiongozi wa DA katika jimbo ya Eastern Cape, jimbo ambali linashika nafasi ya
pili kwa kukaliwa na wazungu wengi nchini humu. Ni kiongozi anayeheshimika sana
ndani ya chama chake na bungeni pia.
Bw. Trollip
pia anatajwa kama mtu makini ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa siasa za Rais
Jacob Zuma kwa hoja zenye mantiki na sio bla bla. Amekuwa akichukuliwa na wafuasi wa DA ambao ni weuzi, kama mtu
anayeweza kuleta mabadiliko ndani ya chama. Hizi ndizo sifa kubwa za Bw.
Trollip katika safari yake ya kutetea kiti chake cha uongozi wa kambi ya
upinzani bungeni hapa Afrika Kusini.
Kwa upande
wake Lindiwe ni binti ambaye ni machachari katika siasa za nchini humu.
Ameingia bungeni mwaka 2009 akitokea jimbo la Kwa Zulu Natal, jimbo ambalo lina
mchanganyiko wa weusi wengi pamoja na weupe katika maeneo ya mijini kama Durban
na miji mingine. Lindiwe ni mmoja kati ya wabunge wanne wenye umri mdogo kuliko
wabunge wengine wote katika bunge la Afrika Kusini.
Kwa sasa
Lindiwe ndie msemaji mkuu wa chama cha DA. Amepewa nafasi hii ya usemaji wa
chama kutokana na upeo wake mkubwa wa kuchanganua mambo kwa hoja zilizojengeka,
kujiamini kwake, na umakini mkubwa katika kujieleza. Pamoja na umri wake mdogo,
Lindiwe ni msichana anayejiamini na kusimama kidete na bila uoga kuitetea hoja
yoyote anayoona ina maslahi kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Katika
uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Mei 18 mwaka huu, mabango ya chama
cha DA nchini kote yalipambwa zaidi na picha za Lindiwe, kiongozi wa DA Bi.
Hellen Zille pamoja na Meya wa jiji la Cape Town mwanamama Patricia De Lille.
Akinamama hawa watatu ni kama roho ya DA kwa sasa na wana ushawishi mkubwa
katika kambi ya upinzani kuliko ushawishi walio nao wanaume.
Wabunge hawa
wawili wa chama hiki kikuu cha upinzani (ambacho daima nakifananisha na
CHADEMA), ndio watakaokabana koo alhamisi ambapo mmoja wao ndie atachukua
jahazi la kuwa kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni. Kampeni kali
zinaendelea hivi sasa katika kutafuta ushawishi na uungwaji mkono katika
uchaguzi huo.
Hata hivyo,
Lindiwe, binti toka kabila la wazulu, anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa na
kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka kidedea katika uchaguzi huo. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba, hadi sasa majimbo matatu ya Kwa Zulu Natal, Limpopo na
Mpumalanga, tayari yametangaza rasmi kumuunga mkono binti huyu katika uchaguzi
huo kati ya majimbo tisa yaliyopo nchini humu.
Mbali na
kuungwa mkono na wabunge wanaotoka katika majimbo haya, Lindiwe anapigiwa
chapuo kubwa na kiongozi mkuu wa DA Helen Zille, na ukaribu wake na kiongozi huyo,
unaweza kuwa moja ya kigezo cha kumfanya ashinde kirahisi nafasi hiyo nyeti
katika siasa za Afrika Kusini.
Hata hivyo
ukaribu wake na Zille pia unatumiwa kama kigezo na wapinzani wake kwamba
atakuwa kibaraka wa kiongozi huyo mzungu wa DA katika uongozi wake ndani ya
bunge. Mbali na sababu hiyo, umri wake mdogo unatumika pia kumuona kama binti
ambaye hajakomaa ipasavyo katika ulingo wa siasa kuweza kupambana na wakongwe
waliosheheni ndani ya chama tawala ANC.
Lindiwe
amekuwa akipambana na vikwazo hivyo, na bado ushawishi alionao hata kwa wabunge
wenzie 82 wa DA, unampa matumaini makubwa ya kutwaa nafasi hiyo. Si yeye tu,
bali hata wadadisi wa maswala ya siasa nchini humu, wana matarajio makubwa kuwa
Lindiwe ndie atakayetwaa nafasi hiyo na hivyo kuanza kwa mabadiliko ndani ya
chama, na kuondoa ile dhana kwamba chama hicho cha upinzani ni cha wazungu,
propaganda inayoshabikiana na ile inayodai kuwa CHADEMA ni chama cha watu wa
kaskazini.
Ukweli ulio
wazi ni kwamba mchuano ni mkali na lolote laweza kutokea. Itakapotokea Lindiwe
amechaguliwa kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani katika bunge la Afrika Kusini,
itakuwa ni historia ya aina yake. Kwanza atakuwa ni kijana mdogo kuwahi
kuongoza kambi ya upinzani ndani ya bunge, na pia binti mdogo kuwahi kushika
wadhifa huo.
Nimeamua
kulinganisha umahiri alionao Lindiwe na ule alionao Halima Mdee, mbunge wa Kawe
kupitia CHADEMA. Halima ni mmoja wa wabunge wanawake vijana na wanaojiamini
ukilinganisha na wengine iwe ni katika chama tawala ama katika kambi ya
upinzani.
Halima Mdee
ni mbunge ambaye yuko tayari kutetea hoja yake kwa hali na mali bila kuogopa
ama kumuonea mtu haya. Kana kwamba haitoshi, Mdee ni mbunge makini, hakurupuki,
hujua namna bora kupanga hoja zake na kuzitetea. Na zaidi ya yote, huyu ni
mbunge asiyetegemea kubebwa na ndio maana aliamua kwenda kupigana jimboni
kuwania ubunge badala ya kutegemea tena viti maalum.
Kama ilivyo
kwa Lindiwe, Halima Mdee ni mbunge msomi pia. Licha ya kuhitimu shahada yake ya
kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es salam, Mdee alikuja hapa Afrika Kusini kwa
masomo zaidi. Hali hii imempanua mawazo zaidi katika ujengaji na utetezi wa
hoja zake, na haikuwa ajabu pale wananchi wa Kawe walipoamua kumpa kura nyingi
katika uchaguzi mkuu mwaka jana.
Ni kutokana
na sifa hizi, na kutokana na kufanana kwake kwa kiasi kikubwa na Lindiwe
Mazibuko wa DA, ndio maana nimeeleza hapo mwanzo kuwa natamani sana kumuona
Halima Mdee akiwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni. Uongozi wake utaleta
changamoto za aina mbalimbali katika demokrasia yetu na siasa zetu za Tanzania.
Kwanza naamini si mtu wa kubebwa, sio mwoga, sio mbabaishaji, sio mnafiki, ni
mjuzi katika kujenga na kutetea hoja, na zaidi ya yote ni mwanadada
anayechipukia katika siasa za Tanzania.
Ninachojiuliza
sana ni kwamba, je, demokrasia hiyo ya kukubali mtu kama Halima Mdee kuwa
kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, na wabunge kama Zitto Kabwe, Tundu
Lissu, Freeman Mbowe na wengineo kuwa chini ya uongozi wake tunayo kweli katika
vyama vyetu vya siasa? Nauliza tu!